Mzungu mmoja alikua na mtaji wa shilingi Milioni moja na akataka kufanya biashara itakayompa faida kubwa kwa kipindi kifupi. Akaenda kwenye kijiji kimoja akawaambia wanakijiji ananunua Ngedere. So kila mwenye ngedere amletee atamnunua kwa sh.10,000/= kwa ngedere mmoja.



Wanakijiji wakachangamkia fursa. Wakakusanya ngedere kwenda kuuza kwa mzungu. Mzungu akanunua ngedere 50 kwa laki 5. Mara ngedere wakaisha. Mzungu kuona ngedere wamepungua akapandisha dau. Ngedere mmoja sasa atamnunua kwa sh.15,000/=. Wanakijiji wajatafuta ngedere wakakosa. Akapandisha dau hadi 20,000/=. 


Kwa tamaa ya fedha wanakijiji wakatafuta ngedere wakapata 20. Mzungu akalipa jumla ya sh.laki 4, yani 20,000/= kwa kila ngedere. Mzungu akawa tayari amekusanya ngedere 70 na amebaki na laki moja. Akatangaza sasa atanunua ngedere kwa sh.30,000/=, wanakijiji wakapagawa. Wakatafuta ngedere wakakosa. Mzungu akapandisha dau kuwa 40,000/= bado ngedere wakakosekana. 

Sasa akafikisha dau la 50,000/= wanakijiji kwa tamaa ya fedha wakatafuta na wakafanikiwa kupata ngedere wawili. Mzungu akawanunua na kufikisha ngedere 72. Mpaka mda huo mtaji wa mzungu ulikua umeisha. Lakini akazidi kutafuta ngedere. Sasa akapandisha dau kuwa 70,000/= kwa ngedere mmoja. Wanakijiji macho yakawatoka. Wakatafuta ngedere wakakosa. 

Mzungu akapandisha dau kuwa 100,000/= kwa ngedere mmoja, wanakijiji mate yakawatoka. Tamaa ya fedha ikawakaba. Wakahangaika wee wakakosa ngedere hata mmoja. Mzungu kuona hivyo akapandisha bei kuwa 150,000/= kwa ngedere mmoja lakini bado ngedere wakakosekana. 

Akafikisha sh.200,000/= lakini hakupatikana ngedere hata mmoja. Sasa akaamua kupandisha bei hadi 300,000/= kwa ngedere mmoja.
Wanakijiji wakawaka tamaa. Kufikia hapa wakashindwa kuvumilia. Wakaamua kusaka ngedere kwa kwa udi na uvumba. Usiku na mchana.

Wakakesha msituni lakini hawakuambulia hata ngedere mmoja. Wakasikia kwenye kijiji cha jirani kuna mzee anauza ngedere. Wakaenda kijiji cha pili wakakuta ngedere wengi. Wakauliza bei, yule mzee akajibu ni laki mbili kwa kila ngedere.

Kwa kuwa yule mzungu aliwaambia atanunua kwa laki tatu wakaona ni biashara nzuri ikiwa watanunua kwa 200,000/= wakamuuzie yule mzungu kw 300,000/= watapata faida ya 100,000/= kwa kila ngedere. Lakini hawakuwa na fedha. Wengine wakaaenda kukopa na wengine wakauza mali zao kama nyumba na ardhi ili wapate mtaji wa kufanya biashara ya ngedere.

Wakanunua ngedere wote kwa yule mzee, wakaenda nao kijijini. Sasa wakawa wanamngojea mzungu ili aje kununua kwao. Wakasubiri siku ya kwanza hawakumuona, siku ya pili, ya 3, mara wiki, mara mwezi, mara mwaka... hawakuona mzungu wala mchina.


Unajua Kilichotokea.?!

Wale ngedere waliokuwa kijiji cha pili ni wa yule mzungu. Alikua anawanunua kwa wale wanakiiji anakwenda kuwahifadhi kijiji cha jirani kwa yule mzee.

Kichwani alijua kabisa ipo siku ngedere wataisha na ataanza kuwauzia walewale wanakijiji bila wao kujua, tena atauza kwa bei kubwa. Yeye alitumia milioni moja kununua ndedere 72.... sasa amekuja kuwauzia wanakijiji walewale kwa laki 2 kwa kila ngedere. Hivyo akapata jumla ya sh.milioni 14.4, Kisha akaondoka na hela zake, akawaachia wanakijiji ngedere wao, madeni na umasikini wa kutupa.

Dhamira ya Kiska hiki.


Kuwa makini sana na maamuzi unayofanya leo maana yanaweza kukugharimu kesho. Kuwa mvumilivu kuna faida kubwa. Watu wengi hutaka faida ya haraka bila kufikiria hatma yao.

Tumia akili yako vizuri. Mtaji mkubwa ni akili yako si kiasi cha fedha ulichonacho. Mzungu hakuwa na fedha lakini alifanya biashara na kupata faida kubwa kwa kipindi kifupi kwa kutumia akili tu.

Hivo akili yako ndio utajiri wako na ndio umasikini wako. Wanakijiji wameachwa na ngedere wao na umasikini ambao hawakua nao kwa tamaa ya haraka na kukosa akili.